DKT SAMIA:TUNAFANYA UCHAGUZI KWA FEDHA ZETU WENYEWE
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema serikali yake inajivunia kutumia fedha za ndani kuendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu bila kutegemea msaada kutoka mataifa ya nje.
Pia amewaahidi wananchi wa Mkoa wa Manyara kwamba akipewa ridhaa kuongoza tena,serikali yake itafanya jitihada kutekeleza maombi ya wagombea ubunge wa majimbo ya mkoa huo, ambayo hayamo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025 - 2030.
Dkt. Samia ameyasema hayo leo Jumamosi Oktoba 4, 2025 alipohutubia mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika kwenye Viwanja vya Stendi ya Zamani mjini Babati.
Dkt. Samia amesema Serikali ya CCM imejipanga vema na ndio maana imerudi kwa wananchi kuomba ridhaa ya kuongoza tena.
"Kwa hiyo hayo ndiyo mambo tutakayofanya, niwaombe ndugu zangu mstahimili kidogo mambo haya yanataka fedha, na wakati huu tulio nao mnajua fedha imekwenda wapi na tunajivunia sana kwamba kampeni zetu zote, uchaguzi wetu wote tumefanya kwa fedha zetu za ndani hakuna aliyetusaidia, tunajivunia hilo," amesema Dkt. Samia.
Aidha, ameahidi kuwa serikali yake itakaporejea tena madarakani, kipaumbele chake kwenye madini itakuwa kwa wachimbaji wadogo ili kutengeneza ajira za vijana.
Amesema sekta ya madini ni muhimu na moja ya nguzo kuu za kukuza uchumi hivyo serikali yake imejipanga kuyapa thamani madini.
"Najua kuna maeneo ambayo leseni zilishikiliwa na wawekezaji kwa muda mrefu bila kufanya uwekezaji, tumefuta leseni zile na tumegawa maeneo kwa wachimbaji wadogo. Kwa hiyo tunakwenda kufanya hivi, tukishapima tukabaini maeneo, wachimbaji wadogo ndio kipaumbele chetu namba moja," ameahidi Dkt. Samia.
Amesema ili kuendelea kuikuza sekta hiyo, serikali imejenga kituo cha pamoja cha uuzaji wa pamoja wa madini ya tanzanite Mererani wilayani Simanjiro ili kuhakikisha biashara inafanyika.
"Vilevile tulifanya mnada wa kwanza wa Tanzanite kulekule Mererani na mnada ule ulikwenda vizuri sana na jina la Tanzania kwenye madini haya (Tanzanite ) lilikwenda juu sana," alieleza Dkt. Samia.
Ameongeza kuwa katika sekta ya utalii, licha ya kupanga kuongeza watalii katika hifadhi za Ziwa Manyara na Tarangire, pia wanakusudia kuongeza idadi hiyo ya watalii nchi nzima.
Akizungumzia changamoto ya mgogoro kati ya Pori la Akiba la Mkungunero na vijiji Wilaya za Simanjiro na Kiteto, amesema licha ya kuweka mipaka bado wananchi walikuwa wakiingia kwenye hifadhi, kufuata huduma muhimu ya maji na maeneo ya kufanyia kazi zao.
"Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, tumeelekeza kuhakikisha vijiji vilivyo jirani na hifadhi vinapata maji ya kutosha... watafanya kazi (Wizara ya Maliasili na Utalii) na Wizara ya Maji kuhakikisha maeneo yale yanapata maji ya kutosha na hili la maeneo ya kufanyia shughuli zao tunakwenda kulifanyia kazi ili hifadhi iendelee na shughuli zao na wananchi waendelee na maisha yao," amesema.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa urais wa CCM ameshuhudia wanachama watatu (3) kutoka vyama vya upinzani,mmoja ni kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na wawili wa ACT Wazalendo wote wa Mkoa wa Manyara, wakihamia CCM.
Wanachama hao ni aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Bw. Olekai Letion Laizer, aliyekuwa Katibu wa Ngome ya Vijana ACT Wazalendo Simanjiro, Bw. Daniel Lucas na Bw. Abubakari Abdalah, aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Babati Mjini na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho.
Wakizungumzia sababu za kuhamia CCM, wanachama hao wamesema kuwa ni kutokana na kazi kubwa ya kuleta maendeleo kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla, lakini kuepukana na upinzani usio wa staha wenye kupandikiza chuki, kuhamasisha vurugu, kebehi na matusi na wenye kuweka mbele maslahi binafsi badala ya taifa.