CCM - Chama Cha Mapinduzi
Muda Wa Kazi: 24/7

Habari na Matukio Mbalimbali


UCHAGUZI UVCCM SIMIYU UMEFUTWA, MCHAKATO WA UNEC ARUSHA NA MBEYA UMESIMAMISHWA, MKOA WA MAGHARIBU UCHUNGUZI UNAENDELEA

alternative

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Uchaguzi wa ndani ya chama unaoendelea katika ngazi ya mikoa, ametangaza kufutwa uchaguzi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Simiyu, kusimamishwa kwa mchakato wa uchaguzi kwenye nafasi za Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) katika mikoa ya Mbeya na Arusha, na kutuma timu ya uchunguzi kwa ajili ya hatua zaidi kupitia maamuzi ya vikao vya chama. 

Katibu Mkuu Chongolo pia amesema kuwa uchaguzi uliofanyika jana tarehe 20 Novemba, 2022 mkoa wa kichama wa Magharibi, huko Zanzibar, nao umesimamishwa kufuatia kuwepo kwa malalamiko dhidi ya tukio la mmoja wa wanachama kubeba sanduku la kura na kulipeleka eneo la kuhesabia,  hivyo timu ya uchunguzi imetumwa kufuatilia nia hasa ya kitendo hicho, ambapo ripoti itakayoandikwa itasaidia maamuzi ya vikao katika hatua za kuchukuliwa, iwapo ni kubatilishwa au kuacha matokeo yaliyotangazwa jana yaendelee. 

Katibu Mkuu ameyasema hayo leo Jumatatu, Novemba 21, 2022, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa Uchaguzi Mkuu wa Ndani wa CCM, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention, jijini Dodoma, 

Katibu Mkuu Ndugu Chongolo amesema kuwa uchaguzi wa UVCCM Mkoa wa Simiyu umefutwa kutokana na kuwepo kwa tuhuma za rushwa, ambapo tayari timu ya uchunguzi imetumwa mkoani humo kufuatilia jambo hilo kwa kina, ambayo itaandika ripoti kwa ajili ya hatua zaidi.

Aidha, Katibu Mkuu ameongeza kusema kuwa amesimamisha uchaguzi wa nafasi ya Mjumbe wa NEC katika mikoa ya Mbeya na Arusha kutokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali, zikiwemo tuhuma za rushwa, na tayari maeneo hayo pia zimetumwa timu za uchunguzi, kwa ajili ya chama kujiridhisha kabla ya kufanya maamuzi ya hatua zaidi kupitia vikao. 

Ndugu Chongolo amewashukuru na kuwapongeza wanachama wote wa CCM kwa namna wanavyoendelea kushiriki uchaguzi kwa hamasa na mapenzi makubwa kwa chama chao, wakidumisha utulivu mkubwa, licha kuwepo kwa changamoto katika baadhi ya maeneo machache ambapo, amesema Chama kinaendelea kufuatilia kwa makini na ukaribu, kabla ya kuchukua hatua stahiki. Amesisitiza wito kwa wanachama na wote wanagombea kuendelea kuzingatia taratibu za Chama, ikiwemo Katiba, Kanuni, Maadili, Miongozo na maelekezo mbalimbali.

alternative

Maoni & Mawasiliano

Unaweza kuwasiliana na CCM, kwa kutumia anuani hapo chini kwa Maswali yoyote na Maoni.
Chama Cha Mapinduzi, Kuu Street, P.O.Box 50, Dodoma-TZ.
Barua Pepe
Muda Wa Kazi
24/7
Anuani
P.O.Box 50