Thursday, May 23rd

Last update11:41:41 AM GMT

Uanachama

  • PDF

 

WANACHAMA

  1. Kila mtu aliyekuwa mwanachama wa TANU au wa ASP mara kabla ya kuvunjwa kwa Vyama hivyo, na aliyekuwa anatimiza masharti ya Uanachama wake, atakuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi, isipokuwa kama atakataa mwenyewe.

  2. Raia yeyote wa Tanzania mwenye umri usiopungua miaka 18, anaweza kuwa Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi iwapo anakubali Imani, Malengo na Madhumuni ya CCM.

  3. Mtu atakayekubaliwa kuingia katika CCM, au kuendelea kuwa Mwanachama, ni yule anayetimiza Masharti yafuatayo:-

    (1)Kuwa mtu anayeheshimu watu.

    (2) Kuwa mtu anayefanya juhudi ya kuielewa, kuieleza, kuitetea na kuitekeleza Itikadi na Siasa ya CCM.

    (3)Kuwa mtu mwenye kuamini kuwa kazi ni kipimochaUtu,nakuitekelezaimani hiyo kwa vitendo.

    (4)Kuwa mtu anayependa kushirikiana na wenzake.

    (5)Kuwa mtu ambaye siku zote yuko mstari wa mbele katika utekelezaji wa mambo yote ya Umma, kulingana na Miongozo ya CCM.

    (6)Kuwa wakati wote ni mfano wa tabia nzuri kwa vitendo vyake na kauli yake, kuwa mwaminifu na kutokuwa mlevi au mzururaji.

    (7)Kuwa ama Mkulima, Mfanyakazi, au mwenye shughuli nyingine yoyote halali ya kujitegemea.

  4. Mtu atakayetaka kuwa Mwanachama atajaza fomu ya maombi na kuipeleka kwa Katibu wa Tawi anapoishi.

  5. Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Tawi itafikiria na kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu maombi ya Uanachama.

  6. CCM itakuwa na Mpango wa kutoa Mafunzo kwa wanachama wake juu ya Imani, Malengo na Madhumuni ya Siasa ya CCM kwa jumla.

  7. (1) Mtu akikubali kuwa Mwanachama itabidi atekeleze haya yafuatayo:-

(a)Atatoa kiingilio cha Uanachama.

(b)Atalipa ada ya Uanachama kila mwezi isipokuwa kama akipenda anaweza kulipa ada ya mwaka mzima mara moja.

(c)Atatoa michango yoyote itakayoamuliwa.

(2)Viwango vya kiingilio, ada na michango vitawekwa na Halmashauri Kuu ya Taifa.

(3) Uanachama wa mwanachama utakwisha kwa:-

(a)Kufariki.

(b)Kujiuzulu mwenyewe.

(c)Kuachishwa kwa mujibu wa Katiba.

(d)Kufukuzwa kwa mujibu wa Katiba.

(e)Kutotimiza masharti ya uanachama.

(f)Kujiunga na Chama kingine chochote cha siasa.

 

(4) Mwanachama ambaye uanachama wake unakwisha kwa sababu yoyote ile hatarudishiwa kiingilio alichokitoa, ada aliyotoa wala michango

yoyote aliyoitoa.

(5)Mwanachama aliyeachishwa au kufukuzwa Uanachama akitaka kuingia tena katika CCM, itabidi aombe upya, na atapeleka maombi yake hayo ama katika Halmashauri Kuu ya Wilaya ama kikao kilichomwachisha au kumfukuza Uanachama.

(6)Mwanachama aliyejiuzulu akitaka kuingia tena katika CCM ataomba upya kwa kufuata utaratibu wa kuomba Uanachama kwa mujibu wa Katiba ya CCM.

 

 

HABARI MPYA

You are here Kuhusu CCM Kujiunga na CCM